Thursday , 19th Jun , 2014

Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia tekinolojia ya kisasa ya Biometric Voters Register (BVR) ambapo kila mwenye kadi ya kupigia kura au aliyetimiza umri wa kupiga kura ataandikishwa.

Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi chini Tanzania (NEC) jaji mstaafu Damian Lubuva.

Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstafu Damian Lubuva amesema hayo leo Jijini Dar-es-Salaam na kufafanua kuwa tekinolojia hiyo ni kwa ajili ya kuwa na orodha ya uhakika ya wapiga kura na kwamba haitatumika kwa kupiga kura za kielektroniki yaani Electronic Voting.

Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, jumla ya shilingi bilioni 293 zitatumika kwa ajili ya kununua vifaa vya zoezi hilo vitakavyowasili nchini Septemba mwaka huu, pamoja na kutoa elimu kwa watumishi watakaosimiamia zoezi la uandikishaji litakaloanza mara baada ya kuwasili vifaa hivyo.

Jaji Lubuva ameongeza kuwa tayari taratibu zimekamilika kwa ajili ya kuanza kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaohusika na zoezi la uboreshaji wa daftari hilo ambalo amesema kukamilika kwake kutamaliza lawama zilizodumu kwa muda mrefu kuwa NEC imekuwa ikipendelea wapiga kura wa chama fulani cha siasa.

Mwenyekiti huyo wa tume ya taifa ya uchaguzi amesema watakaoandikishwa watapatiwa kadi zao za kupiga kura mara baada ya kuandikishwa kupitia mfumo huo mpya na kwamba aina ya vitambulisho watakavyopatiwa vitakuwa na ubora wa kisasa ambao si rahisi kwa mtu kughushi.