
Maxence Mello (Kushoto) na Mike (katikati) wakiwa mahakamani leo
Wakili wa Serikali, Mohamed Salum kwa kushirikiana na Mwanasheria Mwandamizi wa mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, Johannes Kalungula wamewapandisha kizimbani washtakiwa hao, wakaunganishwa na kusomewa mashtaka na katika kesi namba 456 na 457 za Mwaka 2017 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba na hakimu mkazi mkuu, Godfrey Mwambapa.
Wakili Salum Alidai kuwa washtakiwa hao kati ya April Mosi na December 13, 2016, eneo la Mikocheni, Wakiwa na Mkurugenzi wa mtandao wa Jamii Media Co.Ltd ambao unaendesha tovuti ya JamiiForums wakijua jeshi la polisi Tanzania linafanya uchunguzi kuhusiana na mawasiliano ya kimtandao yaliyochapishwa katika tovuti yao kwa nia ya kuuzuia uchunguzi huo walishindwa kutekeleza amri ya kutoa taarifa walizonazo.
Aidha washtakiwa hao kupitia kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa wamedaiwa kufanya kosa kama hilo mnamo Mei 10 na Desemba 13, 2016.
Washtakiwa walikana mashtaka yote yanayowakabili na upande wa mashtaka uliiambia Mahakama upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na wakaomba ipangwe tarehe kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.
Mahakimu hao waliwapa dhamana baada ya kukamilisha masharti waliyopewa yakiwemo ya kuwa na wadhamini wawili wanao aminika ambapo kila mdhamini alisaini bondi ya shilingi Milioni 10.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi February 9 na 20 mwaka 2017 ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali.