Tuesday , 24th Jan , 2017

Mmoja wa wasanii wa kundi la 'Yamoto Band'  Enock Bella ameibuka na kukiri kuwa ni kweli walikuwa na tofauti na uongozi wao na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kundi hilo kushindwa kutoa kazi mpya kwa muda mrefu.

Yamoto Band wakiwa na meneja wao, Chambuso (katikati)

Akizungumza kupitia kipindi cha eNewz ya EATV, Enock amesema kwa sasa wamemaliza tofauti zao na kuwataka mashabiki wao kutovunjika moyo kwani kwa sasa wameshamaliza matatizo madogo madogo yaliyokuwepo kati yao na kusema kuwa "Hakuna mbio nyingi zisizo na mapumziko".

Siku za nyuma kidogo kulikuwa na tetesi kuwa kundi la Yamoto Band lilikuwa na tofauti, jambo lililopelekea wasanii hao kutofanya na kutoa kazi zao mpya kwa muda mrefu lakini siku za karibuni alisikika moja ya kiongozi wa Mkubwa na Wanawe Mhe Temba akisema tayari wanataka kuachia kazi mbili za Yamoto Band ambazo mpaka sasa hazijaweza kutoka.

"Unajua hapo awali kidogo ni kweli tulikuwa na mvurugano kidogo kati ya wasanii na uongozi lakini sasa hivi hakuna tofauti yoyote ile na kila kitu kipo sawa kabisa, na upendo uleule na siyo kuvurugana kwamba kusema wasanii walikuwa hawataki au kugombana kabisa, hapana, sababu Mkubwa yeye ndiye aliyetuleta na yeye ndiye atakayetupoteza. Saidi Fella ni mzee wetu hivyo huwezi kusikia hata siku moja kuwa Yamoto Band wamegombana na Fella" alisema Enock Bella 

Enock Bella

Hata hivyo Enock amesema Chambuso kufuta kwenye mitandao kuwa siyo meneja wa Yamoto Band haijawaathiri chochote kwa kuwa umeneja upo ndani ya moyo wake na siyo kwenye mitandao, huku akisema kuwa malengo yao ni kuwa pamoja kwa kipindi chote katika muziki