Friday , 16th Dec , 2016

Vilabu vikongwe nchini vya Simba na Yanga vimeapa kutokuwa na huruma kwa timu yoyote zitakayokutana nayo katika mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara unaoanza kesho Jumamosi (Desemba 17, 2016)

Wachezaji wa Yanga (Kushoto) na wa Simba (Kulia)

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi wa vilabu hivyo, kila mmoja amesema kuwa watahakikisha hawapotezi point katika kila mchezo utakaokuwa mbele yao ili kufukuzia taji la ubingwa msimu huu.

Katibu Mkuu wa Simba Patrick Kahemele amesema licha ya timu hiyo kukabiliwa na mechi nyingi za nje ya Dar es Salaam, wanaamini haitakuwa tofauti kwa kuwa hata nje ya Dar wana mashabiki wengi isipokuwa tofauti iliyopo ni ubora wa viwanja, jambo ambalo kocha wao Joseph Omog analitambua na amelifanyia kazi.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdedith amesema timu yake iko vizuri, na itahakikisha tofauti ya point mbili iliyopo kati yake na Simba inaondoka mapema, na hivyo kuongoza ligi hadi mwisho wa msimu.

Mzunguko huo wa pili unaanza kesho ambapo Yanga itakuwa katika dimba la Uhuru Dar es Salaam ikiwa mgeni wa JKT Ruvu wakati Simba ikiwa Mjini Mtwara tayari kuvaana na Ndanda FC.

Tags: