Baadhi ya wauguzi waliohudhuria sherehe za siku ya wauguzi duniani wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete ameitaka sekta ya utumishi kuhakikisha kuwa watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo wanapandishwa kwa wakati na kama kuna tatizo liwekwe bayana ili lipatiwe ufumbuzi kwa kuwa sio busara kusubiri hadi walazimike kuidai.
Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Arusha Dkt Kikwete amesema inasikitisha kuona watumishi wenye sifa za kupandishwa vyeo hawapandishwi hadi wanafikia hatua ya kudai na kuandika mabango wakati ni haki yao.
Pia Rais kikwete ameelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya waajiri wanaoendelea kuwakandamiza watumishi wenye nia ya kujiendeleza katika mfumo wa kawaida na hata wanapojiendeleza kwa jitihada zao wamekuwa wakiwawekea visa na kuwashusha vyeo , utaratibu aliodai kuwa ni wa kikoloni.
Aidha Rais amesisitiza azima ya serikali ya kuendelea kutatua changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya afya hasa wauguzi ambao ndio wa kwanza kukutana na wagonjwa ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi yao , vitendea kazi na miundombinu.
Awali naibu waziri wa afya Dkt Steven Kebwe ameelezea hatua iliyofikiwa na wizara yake kukabiliana na changamoto za wauguzi ikiwa ni pamoja na kuzijengea uwezo hosipitali za mikoa, wilaya na vituo vya afya ili viweze kukidhi mahitaji.
Katika risala yao watendaji wa sekta ya uuguzi wameendelea kulalamikia changamoto mbalimbali zinazowakabili walizodai kuwa asilimia kubwa ziko ndani ya uwezo wa serikali na hazipaswi kuwepo kama watendaji wanaohusika wangetimiza wajibu wao.
Katika maadhimisho hayo yalioanza kwa maandamano kivutio kikubwa kilikuwa watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu wanaolelewa na shirika la pamoja tuwalee chini ya ufadhili wa (USAID) ambao waliwasilisha kilio chao mbele Rais kwa njia ya nyimbo juu ya ukosefu wa huduma ya afya na kusababisha asilimia kubwa ya washiriki kumwaga machozi hadharani