Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu amewataka wataalamu wa masuala ya maji watafute njia sahihi itakayowezesha kutatua tatizo hilo kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maji vilivyoko.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri wa Maji wa Afrika (AMCOW) ambao unaokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji Afrika.
“Tunategemea baada ya kumazika kwa mkutano huu wataalamu wetu wataondoka na maazimio mazuri ya kumaliza tatizo la maji katika Bara letu kwa kutumia mito na maziwa ili kufikisha maji kwa wananchi,” alisema.
Akizungumzia kwa upande wa Tanzania alisema, suala la maji limepewa kipaumbele hata katika bajeti ya mwaka huu na kwamba Serikali itahakikisha maji yanapatikana katika maeneo yote ili kutimiza sera yake ya kila mwananchi kupata maji umbali usiozidi mita 400.
Kwa upande wake Rais Mstaafu wa Kenya Mwai Kibaki, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa UNESCO kwa ajili ya masuala ya maji Barani Afrika alisema maji ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi, hivyo wataalamu wanatakiwa kuhakikisha huduma hiyo inapatika katika maeneo yote.
Mkutano huo wa siku tano unahudhuriwa Mawaziri wa Maji kutoka nchi 45 za Afrika na unaongozwa na Waziri wa Maji na Mazingira wa Senegal Amadou Mansour Faye ambaye ni Rais wa AMCOW.