Tuesday , 22nd Mar , 2016

Mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Isaya Mwita Charles ameshinda kiti cha Umeya wa Jiji la Dar es Salaam katika uchaguzi wa Umeya uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Theresia Mbando, mgombea wa Chadema Isaya Mwita Charles alipata Kura 84, Iyanga Yusuf Omary wa CCM Kura 67, huku kura saba zikiharibika ambapo kura halali zilikuwa ni 151.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi huo Meya Mteule wa Jiji la Dar es Salaam Mstahiki Isaya Mwita Charles aliyekuwa amejawa na furaha aliwapongeza wajumbe kwa kuwa na imani naye na kumchagua.

Meya Mwita amesema suala kubwa kwa sasa ni kuwahudumia watu wote wa jiji la Dar es salaam ikiwemo kushughulikia suala la bodaboda pamoja na suala la upunguzaji wa foleni ikiwemo ujenzi wa parking ya magari nje ya mji.

Zoezi hilo ambalo hapo awali liligubikwa na utata kwa takiribani miezi mitatu kutoka na mvutano uliojitokeza kati ya chama tawala CCM na vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) lilifanyika chini ya ulinzi mkali wa Polisi.