Tuesday , 1st Sep , 2015

Mkurugenzi wa Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk. Helen Kijo-Bisimba, ametoa wito kwa jamii kuwachukulia binadamu wote ni sawa, na sio kudharau pale wanapoona mwanamke anagombea nafasi za uongozi.

Dk. Kijo-Bisimba ametoa wito huo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Supa Mix kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kuwa jamii itambue kuwa mwanamke ndio kiongozi wa kwanza, kwani hata nyumbani familia inaongozwa na mama ambae ni mwanamke.

“Jamii iendelee kuwatazama binadamu wote ni sawa na waangalie uwezo wa watu walionao, wasiangalie huyu ni mwanaume au mwanamke, wakiona mwanamume au mwanamke mwenye uwezo wamchague bila kujali wale wanaosema hatuko tayari kuongozwa na mwanamke,” alisema Dk. Kijo-Bisimba na kuongeza kuwa “Kunawatu nimewasikia wakiongea vile, jamii ijue kabisa kila siku wanaongozwa na wanawake kwa sababu mama zao ni wanawake”.

Akiongelea suala la wanawake wengi kujitokeza kugombea nafasi za kisiasa mwaka huu, Dk. Kijo-Bisimba amesema kwamba mapambano ambayo wameyafanya kwa miaka mingi sasa yamezaa matunda, na imewapa watu mtazamo tofauti, na pia ni maendeleo makubwa upande wa siasa nchini.

“Hawa wanapojitokeza watoto wakike wanaokuwa wanaona kuwa kumbe masuala haya pia yanawahusu wanawake, na inatupa picha kwamba uwezekano wa kupata viongozi wanawake kwenye hizo ngazi za juu, umeongezeka kuliko huko nyuma,” alisema Dk. Kijo- Bisimba.