Saturday , 27th Jun , 2015

HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE MAADHIMISHO YA KITAIFA YA SIKU YA KUPIGA VITA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI - BAGAMOYO, MKOANI PWANI,TAREHE 26 JUNI 2015

Salamu na Shukrani
Nakushukuru sana Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na waandazi wa shughuli hii kwa kunialika na kunishirikisha katika Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani. Natoa pongezi nyingi kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Eng. Evarist Ndikilo kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hizi.

Baada ya kuona mabango na kusikia kauli kadhaa kutoka wasanii mmejidhihirishia ni jinsi gani mlivyojitayarisha kufanikisha hafla ya leo. Nawapongeza kwa kushirikiana vyema na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kufanikisha maadhimisho haya.

Mwisho nitoe pongezi zangu kwa TAYOA kutokana na ubunifu wao mzuri wa mawasiliano miongoni mwa vijana. Hongereni sana! Hakika mambo yamefana sana.

Aidha, nawashukuru kwa zawadi nzuri ya saa ambayo itakuwa inanikumbusha wakati wa kulala na kuamka.

Kuadhimisha kupiga Vita Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.
Ndugu wananchi;
Kama alivyoeleza Mwakilishi kutoka UNDP, Dkt. Bwijo Bwijo tarehe 26 Juni ya kila mwaka ni siku maalum ya kuadhimisha kupiga vita matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya duniani. Maadhimisho haya hutupa fursa ya kutafakari hatua tunazopiga katika jitihada zetu za kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika jamii zetu na nchi yetu kwa jumla. Katika siku hii pia, pamoja na kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto za mapambano hayo tunapanga mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo kwa ufanisi zaidi.

Tujenge Jamii, Maisha na Utu wetu bila Dawa za Kulevya.
Ndugu wananchi;
Kila mwaka maadhimisho haya yanapofanyika huwepo kauli mbiu ambayo hutoa ujumbe unaosisitiza jambo lililokusudiwa wakati huo. Kauli mbiu ya mwaka huu ya, “Tujenge jamii, maisha na utu wetu bila dawa za kulevya” inatukumbusha sote kukaa mbali na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Dawa za kulevya ni hatari kwa maisha ya mwanadamu, utu wake na ustawi wa jamii yake. Kauli mbiu hii inatutaka tujenge jamii, maisha na utu wetu bila kujihusisha kwa namna yoyote ile na dawa za kulevya.

Dawa za kulevya hazina manufaa yo yote bali hasara tele. Mapambano haya dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanamhusu kila mmoja wetu wadogo kwa wakubwa, viongozi na wananchi wa kawaida, matajiri na maskini, Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kwani athari zake humgusa kila mmoja wetu.

Madhara ya dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Ni jambo lililo dhahiri kuwa dawa za kulevya zina madhara makubwa sana. Matumizi na biashara ya dawa za kulevya inaathiri ustawi wa binadamu. Hudhoofisha afya za watumiaji, na huchochea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI, homa ya ini na mara nyingi husababisha vifo. Hali kadhalika, huchochea rushwa miongoni mwa watumishi wa umma hasa wale wanaotegemewa kuongoza mapambano dhidi yake. Kwa mujibu wa tamko la Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Uhalifu na Dawa za Kulevya alilolitoa tarehe 5 Juni, 2013 kwenye Mkutano wa mwaka wa Vyombo vya Udhibiti wa Dawa za Kulevya uliofanyika Moscow, watu wapatao 200,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Biashara ya dawa za kulevya imeleta changamoto kubwa kwa jumuiya ya kimataifa. Kwa baadhi ya nchi, biashara hii imekuwa ni janga kubwa ambalo limesababisha kuharibika kwa mifumo ya kiutawala na kisheria, uvunjifu wa amani na usalama, kudorora kwa maendeleo ya kijamii na ya kiuchumi. Biashara hii huchochea kuwepo kwa magenge ya kihalifu yanayojihusisha na mauaji, wizi na ujambazi. Hali kadhalika, mapato yake yanafahamika kugharamia shughuli za ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ya fedha haramu, biashara haramu ya silaha na uporaji wa nyara za taifa - vitendo ambavyo ni tishio kwa usalama wa dunia. Hivi basi kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni vita vya haki na ni wajibu kwa kila mtu kushiriki. Lazima tushinde vita hii.

Juhudi za Mapambano Kimataifa
Ndugu wananchi;
Mataifa mengi duniani yametambua madhara ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Pia watu wengi wanauona umuhimu wa kufanya juhudi za pamoja ndani ya nchi, kikanda na kimataifa kukabiliana na uhalifu huu. Matokeo yake ni kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Uhalifu na Dawa za Kulevya. Pia, ni kufanyika kwa operesheni za pamoja za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zinazofanywa na mataifa mbalimbali kikanda na kimataifa. Jambo lingine ni pamoja na kuwepo kwa mikutano ya pamoja kimataifa na kikanda kwa ajili kupanga mikakati ya pamoja.

Naungana na viongozi wenzangu wa nchi mbalimbali duniani na mashirika wa kimataifa katika mapambano haya. Nakemea vikali matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kuwaonya wananchi wajiepushe kabisa kujihusisha nazo. Ni imani yangu kuwa, Watanzania wenzangu mtafanya kila liwezekanalo kujiepusha na kuwaepusha watu wengine hasa vijana na watoto kujihusisha na balaa hili. Watanzania wenzangu tuongozwe na kauli mbiu ya TANU wakati wa kudai uhuru na kujenga nchi inasema, “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu”. Na kwa sasa kauli ya CCM isemayo, ”Umoja ni Ushindi”. Hakika umoja wetu ndio utakaotuhakikishia ushindi katika mapambano haya.

Vyombo vyetu Viko Macho
Ndugu wananchi;
Naomba niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake katika mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa ya kulevya bila kuchoka na bila kigugumizi au ajizi yoyote. Lengo letu ni kudhibiti hali ili kuzuia isizidi kuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa na kubadili mwelekeo ili hatimaye tulikomeshe kabisa tatizo hili hapa nchini. Kwa ajili hiyo, tumekuwa tunafanya mambo makuu matatu.

Kwanza, kuimarisha vyombo vya dola vinavyoongoza mapambano dhidi ya uhalifu huo. Tunayo Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ambayo imefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii kujiepusha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Tumeendelea kuijengea uwezo Tume hiyo pamoja na Jeshi la Polisi ambalo ndilo linalokamata wafanya biashara na watumiaji na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria. Pamoja na hayo nikaamua kuunda Kikosi Kazi kilichojumuisha Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya. Kikosi Kazi hicho kimefanya kazi kubwa na nzuri. Kimeongeza nguvu na uwezo wa kupambana na uhalifu huu na wahalifu wanaojihusisha na biashara hii haramu na wanaotumia dawa za kulevya. Wafanya biashara wengi wadogo, wa kati na wakubwa wamekamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Ukamataji wa Dawa za Kulevya nao umeongezeka sana na hivyo kunusuru taifa na hata dunia na madhara ambayo dawa hizo zingefanya. Tumezisikia takwimu zilizotolewa na Ndugu Keneth Kaseke, Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya.

Hiki ni kiwango kikubwa cha mafanikio hivyo vyombo vinastahili pongezi nyingi kutoka kwetu sote. Takwimu hizi zinatuonesha kuwa tatizo ni kubwa hivyo lazima tuwe katika hali ya tahadhari wakati wote (saa 24 kwa siku zote saba za wiki).

Pili, ili kuongeza nguvu, mbinu na maarifa ya kupambana na uhalifu huu wa hatari na kutisha, tumetunga Sheria (mpya) ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2015. Sheria hii imejengeka juu ya hali ilivyo sasa katika mapambano haya. Mafanikio na changamoto zilizopo imezingatiwa hivyo ni Sheria inayoimarisha mafanikio tuliyoyapata na kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo. Sheria inaunda chombo maalum cha kupambana na Dawa za Kulevya. Chombo hiki kitakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya nchini. Kimepewa mamlaka ya kupeleleza, kupekua na kukamata wafanya biashara na watumiaji wa dawa za kulevya. Nina imani kubwa kwamba chombo hiki kitasaidia sana kupunguza tatizo hili nchini. Natanguliza kuwaomba wananchi na vyombo vingine vyote vya Serikali kutoa ushirikiano wa kutosha kwa chombo hiki mara kitakapoanza kazi ili tuweze kulinusuru taifa letu na tatizo hili.

Huduma za Matibabu
Ndugu wananchi;
Kwa kuzingatia hekima na busara za usemi wa Wahenga, ”Kinga ni bora kuliko tiba”, mkakati wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya unasisitiza sana kuelimisha jamii kuhusu kuepukana na kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa wale waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya, mkakati ni wa Serikali kuendeleza jitihada za kuwapatia ushauri nasaha na matibabu. Hilo ndilo jambo letu la tatu. Kwa sasa huduma hizi zinapatikana katika vitengo vya magonjwa ya akili katika hospitali za baadhi ya mikoa na wilaya hata nchini. Hata hivyo, idadi ya watumiaji wanaopata nafasi ya kupata huduma za tiba bado ni ndogo sana. Takwimu zinaonesha kuwa kuna watumiaji wa heroin wanaokadiriwa kuwa kati ya 200,000 na 425,000 nchini. Idadi ya watumiaji wa heroin wanaopata matibabu kwa kutumia tiba ya methadone mpaka kufikia Mei, 2015 ni 2,300 tu. Watu hawajitokezi kwa wingi. Tafadhalini ndugu zangu jitokezeni mpate uponyaji.

Ninaiagiza mikoa yote hasa ile yenye matatizo makubwa ya matumizi ya dawa za kulevya hususani Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Pwani na Shinyanga kuchukua hatua thabiti za kuanzisha na kuendeleza huduma hizi. Lazima tutambue pia, kwamba hakuna Mkoa ambao uko salama, tofauti ni kiwango cha athari. Hivyo basi kila Mkoa ujiandae ipasavyo. Tahadhari kabla ya hatari. Nawataka Viongozi wa Mikoa na Wilaya kote nchini wafuatilie utekelezaji wa jambo hili. Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya ziliweke suala la dawa za kuleya kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyao.

Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wale wote waliosaidia katika kuanzisha na kuendeleza huduma ya methadone na huduma nyingine za matibabu nchini. Niruhusuni nitoe shukrani maalum kwa Rais Barack Obama na Serikali ya Watu wa Marekani kwa msaada mkubwa wnaotupatia kwa upande wa matibabu.

Tusiharibu Taswira ya Nchi yetu
Ndugu wananchi;
Narudia kuelezea masikitiko kuhusu baadhi ya Watanzania wenzetu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nje ya nchi. Hawa ni chachu ya kuendelea kwa tatizo hapa nchini. Pia, wanaharibu taswira nzuri ya nchi yetu kimataifa na kuhatarisha maisha yao. Zipo taarifa kuwa kati ya Januari 2012 na Desemba 2014, kwa mfano, jumla ya Watanzania 111 walikamatwa kwa kujihusisha biashara hiyo katika nchi za Brazil na China. Hii ni fedheha kubwa. Pia, naomba niwakumbushe na kuwatahadharisha kuwa baadhi ya nchi hutoa adhabu kali ikiwemo ya kifo kwa watu watakaokamatwa na kutiwa hatiani. Mfano mmoja wapo ni wa yale yaliyotokea Indonesia kati ya Januari na Aprili 2015 ilipowanyonga wasafirishaji wa dawa za kulevya 12 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo za Afrika. Nchi hiyo ilikataa maombi ya nchi zao kutaka adhabu hiyo isitekelezwe dhidi ya raia wao.

Akitetea uamuzi wa nchi yake Mwanasheria Mkuu wa Indonesia Muhammad Prasetyo baada ya hukumu kutekelezwa alisema;
‘Tunapigana vita dhidi ya uhalifu wa kutisha wa dawa za kulevya ambao unatishia mustakabali wa taifa letu. Napenda kusema kwamba kuua si jambo jema, si jambo la kufurahisha. Lakini lazima tufanye hivyo kwa ajili ya kuliokoa taifa na hatari ya dawa za kulevya. Hatufanyi uadui na nchi ambazo raia wake walihukumiwa kifo.’
Nawaasa Watanzania wenzangu watambue ukweli huu na kuachana na biashara ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi yetu. Ni hatari kwao na taifa pia. Ingawa hapa nchini adhabu ya kifo haitolewi kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya 2015 ambayo itaanza kutumika hivi karibuni inatoa adhabu kali hadi kifungo cha maisha.

Tahadhari Dhidi ya Matumizi ya Shisha
Ndugu wananchi;
Kwa masikitiko makubwa, Serikali imepokea malalamiko mengi kuhusu matumizi ya shisha nchini. Matumizi haya yameenea kwa haraka katika maeneo mengi ya starehe na huwavutia vijana wengi wa kiume na wa kike. Watumiaji wa kilevi hiki huonyesha dalili zinazofanana na za utumiaji wa dawa za kulevya. Hivyo, kuna hofu kuwa kilevi hiki kinachanganywa na dawa za kulevya. Kama hiyo ni kweli ni jambo hili ni la kusikitisha sana, halikubaliki na kwamba hatuna budi kuhakikisha kuwa haliachwi kuendelea. Nichukue nafasi hii kuziagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kupata majibu yatakayosaidia kutatua tatizo hili na hatimaye kuinusuru jamii yetu.

Tusiruhusu Rushwa Ijipenyeze
Ndugu wananchi;
Mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya si lelemama. Kuna changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na vishawishi vya rushwa. Vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu vinachangia sana katika kurudisha nyuma mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya. Natoa agizo kwa mamlaka husika kuhakikisha kuwa suala la rushwa linadhibitiwa kikamilifu katika mapambano haya kwa kuwachukulia hatua stahiki wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Mjitokeze kwa Wingi Kujiandikisha
Ndugu wananchi;
Wote mnatambua vema kuwa mwaka huu tutakuwa na uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali katika Taifa letu. Nawaasa wananchi wenzangu muendelee kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura. Wakati wa kupiga kura utakapofika, mtumie haki yenu ya kikatiba kuchagua viongozi waadilifu ambao kwa namna yoyote ile hawajihusishi na biashara au matumizi ya dawa za kulevya. Aidha, nawaasa wazazi na walezi, viongozi wa dini, viongozi wa asasi za kijamii, watambue kuwa hivi ni vita vyetu sote. Tatizo la dawa za kulevya likiachiwa bila kudhibitiwa kwa dhati litaleta maafa makubwa kwa kizazi cha sasa na kijacho. Kwa sababu hiyo, tunao wajibu wa kupambana kila mtu kwa nafasi yake. Tuwalee watoto wetu kwa misingi ya maadili mema ili kujenga Taifa lisilokuwa na matumizi wala biashara ya dawa za kulevya. Inawezekana Timiza Wajibu wako.

Tujenge jamii, maisha na utu wetu bila dawa za kulevya
Asanteni kwa kunisikiliza