
Timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes leo imeanza vibaya mbio za kuwania kombe la CECAFA Chalenji katika michuano inayohusisha timu za ukanda wa Afrika Mashariki na kati, iliyoanza leo nchini Ethiopia.
Katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, Zanzibar Heroes imecheza na Burundi ukiwa ni mchezo wa kundi B na kuchapwa bao 1-0 lililofungwa na Didier Kavumbangu dakika ya 39.
Matokeo haya yanaiweka Zanzibar katika wakati mgumu kwani italazimika kushinda michezo yake miwili iliyobaki ili kutinga robo fainali.
Katika kundi hilo, pia kuna timu za Kenya na Uganda ambazo Zanzibar itakabiliana nazo katika mechi zinazofuata.
Katika mchezo uliofuata wenyeji Ethiopia wameangukia pua kwa kuchapwa bao 1-0 na Rwanda, bao likifungwa na Tuyisenge.
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ tayari kimewasili Addis Ababa nchini Ethiopia kikiwa na wachezaji 18 pamoja na vinogozi tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayoanza kutimua vumbi kesho Jumamosi nchini humo.
Kilimanjaro Stars inayonolewa na kocha mkuu Abdallah Kibadeni, akisaidiwa na kocha msaidizi Juma Mgunda, imepangwa katika kundi A, ikiwa na wenyeji timu ya taifa ya Ethiopia, Rwanda, pamoja na Somalia.
Wachezaji waliosafiri na timu hiyo ni magolikipa Ally Mustafa na Aishi Manula, walinzi Shomari Kapombe, Kessy Radmahani, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Ishaka, Salim Mbonde na Kelvin Yondani.
Wengine ni viungo Himid Mao, Salum Abubakar, Jonas Mkude, Salum Telela na Said Ndemla, huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Malimi Busungu, Elias Maguri, Saimon Msuva, Deus Kaseke na nahodha John Bocco.
Stars itacheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Somalia siku ya Jumapili katika uwanja wa Addis Ababa.