Friday , 14th Dec , 2018

Kocha mkuu wa vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, Mwinyi Zahera ametoa masharti kwa shirikisho la soka nchini TFF, kuwa libadilishe ratiba ya baadhi ya michezo  ili kuweza kuwapa nafasi wachezaji kupumzika.

Kocha Mwinyi Zahera

Kocha huyo raia wa DR Congo ameweka wazi suala hilo kuwa ni kutokana na kuwepo kwa mechi nyingi za michuano mbalimbali ikiwemo ligi kuu, kombe la Mapunduzi na kombe la shirikisho nchini.

''Naomba wakubwa watazame ratiba ya hii michuano inayokuja ya Mapinduzi na kombe la shirikisho huwezi kuchezesha wachezaji kiasi hicho, waende Mbeya kombe la shirikisho kisha wakacheze ligi kuu na bado waende Mapinduzi, vinginevyo nitapeleka vijana wa U20 wakacheze'', amesema Zahera.

Zahera amesisitiza kuwa shirikisho linatakiwa kutazama upya ratiba ya ligi kuu ili kuipa timu hiyo nafasi ya kupangilia ushiriki wake kwenye michuano inayokuja hapa karibuni.

Hivi karibuni Zahera alilalamikia ratiba ya Simba na Mtibwa Sugar kutocheza mechi za ligi kuu kwasababu ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika na kombe la shirikisho.