Monday , 20th Jun , 2016

Yanga SC imeanza vibaya mechi za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia.

Beki Yassine Salhi alizifumania nyavu katika dakika ya 20 akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji Ismail Belkacemi.

Beki wa Yanga Haji Mwinyi alipewa kadi nyekundu dakika ya 90 kufuatia kuwa alishachukua kadi nyingine ya njano kabla baada ya kucheza rafu katika mchezo huo.

Matokeo hayo yanaifanya MO Bejaia ishike nafasi ya pili katika kundi hilo, nyuma ya TP Mazembe ambayo iliifunga Medeama ya Ghana 3-1 katika mchezo wa kwanza mjiji Lubumbashi Jumapili, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu.

Mechi zijazo za kundi hilo, Yanga watakuwa wenyeji wa Mazembe Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Medeama wakiikaribisha Mo Bejaia.

Kikosi kamili cha Yanga kinachoanza ni; Deogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua/Mwinyi Hajji dk32, Kelvin Yondani, Vicent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe/Matheo Anthony dk85 na Deus Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk75.

MO Bejaia; C. Rahmani, A. Messaoudi, A. Lakhdari, S. Baouali, S. Khadir, Y. Salhi/ M. Betorangal dk71, S. Benali, S. Sidibé, M. Ferhat/A. Mouhli dk87, M. Athmani na I. Belkacemi/ B. Bendjelloul dk79.