Sunday , 29th Jan , 2017

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara leo wanashuka dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kupambana na Mwadui FC ya Shinyanga huku wakimkosa beki wake Andrew Vincent 'Dante'.

Dante

 

Meneja wa Yanga Hafeedh Saleh amesema, kwa taarifa za daktari, Dante hatakuwepo katika mchezo huo kutokana na majeraha aliyonayo ambayo yanamzuia kuonekana katika mchezo huo.

Hafidh amesema mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma naye hatakuwepo katika mchezo huo kwani yuko kwao kwaajili ya matatizo ya kifamilia huku beki Vincent Bossou aliyekuwa katika timu yake ya taifa ya Togo akishiriki fainali za mataifa ya Afrika nchini Gabon akitarajiwa kuwasili siku yoyote kuanzia leo.

Mchezo wa leo ni fursa kwa Yanga kukaa kileleni endapo itapa ushindi mara baada ya mahasimu wao Simba kuambulia kichapo katika mchezo wa jana dhidi ya Azam FC kwani hadi sasa Yanga ina point 43 wakati Simba ikiwa na point 45.

Katika michezo inayopigwa leo, Yanga watakuwa wenyeji wa Mwadui FC, Kagera Sugar nao watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar na JKT Ruvu wataikaribisha Stand United huku Ndanda FC ikikwaruzana na Majimaji FC, ukiwa ni mchezo ulioahirishwa siku ya jana.