Thursday , 10th Sep , 2015

Michuano ya Kombe la Shirikisho (FA CUP) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba Mwaka huu mpaka Mei mwakani kwa kushirikisha vilabu 64 vya ligi kuu, ligi daraja la Kwanza na ligi Daraja la pili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Shirikisho la Soka nchini TFF Geoffrey Nyange Kaburu amesema michuano hiyo itakayoshirikisha timu 16 za Ligi kuu, 24 Daraja la kwanza na 24 Daraja la Pili yataendeshwa kwa njia ya mtoano ambapo wiki ya kuanza kwa michuano hiyo hakutakuwa na michuano ya Ligi kuu.

Kaburu amesema, mshindi wa kombe hilo atapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 2017.

Kwa upande wake Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema, duniani kote maendeleo ya soka yanatokana na kuwepo na mashindano mbalimbali yakiwemo ya Kombe la Shirikisho la nchi, ambayo yanashirikisha na klabu za chini hadi zile zinazoshiriki Ligi Kuu.

Malinzi amesema, amefurahi kuona klabu ya Daraja la Pili inashinda kombe hilo kwani duniani kote kombe hilo lipo na klabu za chini zimekuwa zikiwapiga ‘visu’ wale wakubwai.

Mara ya mwisho kombe la FA lilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu Stars ya Pwani ikaibuka bingwa baada ya kuifunga Baker Rangers ya Magomeni kwenye fainali ambapo bingwa wa kwanza wa kombe la FA enzi hizo likiitwa Kombe la FAT ilikuwa Yanga SC mwaka 1967 na michuano hiyo haikufanyika tena hadi 1985 Majimaji ya Songea ilipotwaa Kombe.

Kombe la FAT likayeyua tena kabla ya kurejea miaka 10 baadaye, 1995 na Simba SC ikatwaa ubingwa kabla ya kupokonywa na Sigara mwaka 1996, ambao nao walilitema kwa Tanzania Stars mwaka 1997 iliyofanikiwa kulitetea 1998 kabla ya kupokonywa na Yanga SC 1999.

Ubingwa wa FA mwaka 2000 ulikwenda kwa Simba SC, waliopokonywa na Yanga SC mwaka 2001 kabla ya JKT Ruvu kuwa bingwa wa mwisho wa mashindano hayo mwaka 2002.