Monday , 17th Dec , 2018

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo amewapa changamoto vijana kwa kuwakumbusha juu ya kutumia fursa za uwekezaji hususani kwenye ardhi ambapo amehoji juu ya idadi ya vijana ambao wamepitia sheria ya ardhi ya mwaka 1999.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo (aliyesimama) akiongea kwenye mkutano huo.

Akiongea leo kwenye moja ya mikutano ya kujadili fursa za vijana Jokate amesema vijana wengi hawapati taarifa sahihi ndio maana wanakosa baadhi ya vitu ambavyo ni haki yao na pengine wangeweza kuvifanya na vikawakwamua kiuchumi.

''Vijana wengi hawajui hata jinsi ya kupata ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwa mfano wangapi wamepitia sheria ya ardhi na 4 na 5 za mwaka 1999?'', amehoji Jokate.

Hata hivyo Jokate amesisitiza kuwa maafisa maendeleo ya jamii na maafisa vijana wana kazi ya ziada ya kufanya na kuweka ubunifu zaidi katika kuwafikia na kuwawezesha vijana wengi zaidi.

Aidha Jokate ameongeza kuwa hakuna ambaye alikuwa anadhani Dar es salaam ingekuwa hivi miaka 70 iliyopita hivyo hata Kisarawe itabadilika lakini inahitaji ushiriki wa vijana ili kuweza kuibadilisha.