Wednesday , 1st Jun , 2016

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa Klabu ya Young Africans imesema mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Jumatatu Juni 6, 2016 saa 10:00 jioni.

Hadi sasa wanachama tisa (9) wamechukua na kurejesha fomu. Wanachama hao ni Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa.

Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' Omari Said kutoka Zanzibar ambao wanawania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Uchaguzi wa Yanga unatarajiwa kufanyika Juni 25, 2016.

Fomu zinapatikana katika ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. Vilevile utaratibu unafanyika ili fomu ziweze kupatikana katika tovuti ya shirikisho.

Fomu zinapatikana kwa gharama ya Sh 200,000 kwa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti na Sh 100,000 kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji.