Monday , 11th Apr , 2016

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini Tanzania Takukuru imesema imeshaanza uchunguzu kuhusiana na suala la rushwa linaloizunguka Shirikisho la Soka nchini TFF juu ya upangaji wa amatokeo.

Msemaji wa Takukuru Tunu Mleli amesema, tatizo la rushwa halipo katika michezo peke yake hivyo wananchi na wadau wa michezo kwa ujumla wanatakiwa kutoa taarifa kwa haraka pale wanapoona vitendo vya rushwa vinatendeka sehemu yoyote ili wahusike waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

Kwa upande wake aliyekuwa Mjumbe wa bodi ya Ligi Damas Ndumbaro amesema, ushahidi wa sauti uliosikika katika suala la upangaji wa matokeo katika mechi za Ligi Daraja la kwanza ni halali ambao unaweza ukapokewa mahakamani na kumtia mtu hatiani.

Ndumbaro amesema, suala la msingi ambalo mahakama litaangalia ni chanzo au chimbuko na uhalali wake kwani sauti pia inaweza ikatengenezwa ili kuweza kumchafua mtu.

Ndumbaro amesema, waliotajwa katika sauti zile wangejiondoa wenyewe mapema kabla ya kufukuzwa au kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi ili kamati ya utendaji ikae ijadili suala hili.

Ndumbaro amesema, anategemea kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka nchini TFF inatakiwa kutenda haki kwa wahusika wanne waliotajwa katika sauti ile na watu hao wanatakiwa wakae pembeni wakati uchunguzi unafanyika.

Suala zima la upangaji wa matokeo ya Ligi Daraja la Kwanza limevikuta vilabu vya Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) ambapo Kamati ya Nidhamu ya TFF ilitoa adhabu ya kushushwa daraja mpaka igi daraja la pili (SDL) msimu ujao.