Wednesday , 19th Aug , 2015

Chama cha Waandishi wa Habari za michezo mkoani Arusha (TASWA) kimeandaa tamasha kubwa la michezo lengo ikiwa kuhamasisha uchaguzi wa amani,huru na wa haki hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Katibu wa Taswa Jijini Arusha,Mussa Juma akiongea na waandishi wa habari kuhusiana Tamasha la Taswa.

Mwenyekiti wa TASWA, Musa Juma akizungumza na Waandishi wa Habari amesema kuwa tamasha hilo linatarajia kufanyika Agosti 29 mwaka huu katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid huku likiwaunganisha wanahabari kushiriki michezo kwa pamoja na familia zao.

Musa amesema kuwa michezo itakayokuwepo ni pamoja na mpira wa miguu,mpira wa pete,kuvuta kamba na michezo mingine. Washiriki wakubwa wa tamasha hilo ni wanahabari kutoka mkoa wa Arusha na Dar eslaam, Manyara na Arusha ambapo timu sita zinatarajia kuchuana vikali, hivyo amewataka wanahabari na watanzania wajitokeze kwa wingi katika tamasha hilo.

Kwa upande wao wadhamini wa tamasha hilo kutoka taasisi ya fedha ya FAIDIKA,Elia Mlay amesema kuwa wameamua kufadhili tamasha hilo kwani michezo ni afya,ni burudani na pia hutumika kuwaunganisha watu kote duniani hivyo amewataka vijana kuamka kimichezo ili kukuza vipaji vyao.

Meneja Masoko wa Pepsi Tanzania Lalit Sharma amesema kuwa kwa mara nyingine wamejitokeza kudhamini tamasha hilo kwani wao ni wadau muhimu wa masuala ya michezo nchini na wataendelea kuunga mkono michezo kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanahabari kwani mchezo huo unaongoza kwa kupendwa bara la Afrika na Tanzania pia.

Tamasha la kumi la waandishi wa habari za michezo linatarajia kuwa kiunganishi cha kuwaunganisha wanahabari kujenga umoja na mshikamano thabiti miongoni mwa wanahabari pia kuhimiza uchaguzi huru na wa haki utakaodumisha amani ya nchi.