Friday , 29th Apr , 2016

Kama ilivyokawaida ya michuano ya riadha kwa sasa barani Afrika na duniani kwa ujumla Wanariadha wa Kenya na Ethiopia wamekuwa wakisumbua na kutawala mashindano mbalimbali ya mbio za kimataifa barani Afrika na Duniani kwa ujumla.

Wanariadha wakichuana katika moja ya michuano ya Afrika Mashariki.

Wanariadha wa Kenya wameanza kwa nguvu michuano ya riadha ya vijana waliochini ya umri wa miaka 20 iliyoanza rasmi hii leo katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam mbio ambazo zinashirikisha nchi zaidi ya 11 kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki zikiwemo nchi maarufu kwa mchezo huo kama Ethiopia na Elitrea na wenyeji Tanzania ambao leo hawakufua dafu kwa wenzao hao na kujikuta wakiambulia nafasi za mwisho katika hatua za awali.

Maandalizi ya kutosha na pia uzoefu wa hali ya juu kutokana na kushiriki michuano mingi ya ndani na nje kwa wanariadha wa Kenya imeelezwa kuwa ndiyo chachu ya mafanikio ya wanariadha wao wanaoshiriki michuano ya mbio za vijana kwa nchi za Afrika Mashariki kutawala mbio hizo.

Katika mbio zilizochezwa leo za urefu tofauti kuanzia mita 100 hadi 5000 na zile za kupokezana vijiti Wakenya wameongoza katika kila mbio wakishika nafasi mbili za juu au hata tatu za juu na kuwaacha mbali Watanzania ambao walionekana kukimbia bila malengo kana kwamba walikuwa hawajapata maandalizi ya kutosha ilhali wanashiriki michuano hiyo wakitokea kambini mjini Kibaha mkoa wa Pwani.

Michuano hiyo ambayo imefunguliwa hii leo na Mgeni rasmi Katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel inataraji kushitimishwa kesho kwa fainali zote za mwisho na pengine labda katika fainali hizo wanariadha wetu wanaweza kuinuka na kuambulia chochote.

Wakati huo huo Rais wa Riadha Tanzania ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Simiyu Mh. Anthony Mtaka amesema matokeo ya wanariadha wetu si ya kulaumiwa hasa kutokana na mfumo tulionao sasa wa uteuzi wa wanariadha hao kupitia michuano wanayoshiriki ambayo inakua ikiendeshwa ama kusimamiwa na watu ambao si wanataaluma wa mchezo huo.

Jambo lingine ambalo Mtaka amekiri kuwa limewanyima nafasi wanariadha wetu ni suala la baadhi ya nchi shiriki akitolea mfano wa wazi kwa Wakenya kuwa wamefanya udanganyifu kwakuwaleta baadhi ya washiriki ambao wamezidi umri sahiki wa miaka chini ya 20 ambao wengi hata kwakuwatazama usoni utawabaini kirahisi na wengine wanatambuliaka kwakuwa waliwahi kushiriki miaka mitano iliyopita michuano hiyo na mingine inayozingatia umri.