Nahodha wa taifa stars Mbwana Samatta akitoka ndani baada ya taifa stars kuwasili kutoka Chad.
Kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimewasili Dar es Salaam alfajili ya hii leo, na mara baada ya kuwasili, Taifa Stars walipokewa na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja ambaye aliwapa hotuba fupi ya mapokezi na kuwatia moyo na nguvu kuelekea mchezo wa marudio.
Stars ambayo Jumatano iliwafunga wenyeji wao Chad kwa bao 1-0 katika mchezo wa Kundi G kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Omnisports Idriss Mahamat Ouya mjini D’jamena mara baada ya kuwasili, ilikwenda moja kwa moja kambini, hoteli ya Urban Rose, katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Wachezaji waliowasili na Taifa Stars usiku huu kutoka Chad ni makipa; Aishi Manula na Ally Mustafa ‘Barthez’.
Mabeki; Juma Abdul, Shomary Kapombe, Mwinyi Hajji, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Kevin Yondan na David Mwantika.
Viungo; Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Himid Mao, Mohammed Ibrahim, Ibrahim Hajib, Deus Kaseke, Farid Mussa na Shiza Kichuya.Washambuliaji ni John Bocco, Thomas Ulimwengu na Nahodha Mbwana Samatta.
Wachezaji hao wataungana na wachezaji wengine sita waliobaki kambini Dar es Salaam, ambao ni kipa Shaaban Kado, viungo Ismail Khamis ‘Suma’, Said Ndemla na washambuliaji Elias Maguri, Jeremiah Juma na Abdillah Yussuf ‘Adi’.
Stars inashika nafasi ya tatu katika Kundi G, ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Chad, kufungwa na Misri 3-0 na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria.
Misri inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi nne sawa na Tanzania, lakini ina wastani mzuri wa mabao, wakati Chad inashika mkia haina pointi.
Wakati huo huo EATV Michezo ilitembelea kambi hiyo nakufanya mazungumzo na kocha msaidizi wa stars Hemed Morocco pamoja na nahodha wa timu hiyo Mbwana Ally Samatta ili kujua mikakati ikoje kuelekea mchezo huo dhidi ya Chad.
Wakiongea kwa kujiamni kocha Morocco na nahodha Samatta wamesema watajipanga vema kuhakikisha ushindi mnono unapatikana na pia wanauhakikka kwa sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki basi ni wazi ushindi mkubwa utapatikana.
Aidha kocha Morocco amesema pamoja na stars kushinda mchezo wa awali kwa bao 1-0 bao lililofungwa na nahodha Mbwana Samatta lakini mchezo huo haukuwa rahisi hivyo kwakuzingatia hali hiyo wamejipanga kufanya mabadiliko kiuchezaji hasa kutokana na kuwajuwa wapinzani wao na pia watafanyika kazi kasoro ama mapungufu ya kiufundi katika mchezo wa awali ili wazoe pointi zote katika mchezo wa marudiano siku ya jumatatu .