Tuesday , 9th Jun , 2015

Uongozi wa Shirikisho la Soka nchini TFF umesema utata wa kimkataba uliopo kati ya mchezaji wa Klabu ya Simba Ramadhani Singano Messi na Klabu yake ya Simba utamalizwa katika mkataba mpya utakaosajiliwa na mchezaji huyo katika msimu ujao wa ligi kuu.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Celestine amesema, pande zote mbili zimeeleza kutambua utata uliopo ndani ya mikataba hiyo ambayo iliingiwa katika uongozi uliopita.

Kwa upande mwingine, Mwesingwa amesema maamuzi yaliyotoka yamekubalika kwa pande zote mbili katika utata huo lakini alishindwa kuweka bayana kuwa katika mikataba hiyo upi ulio sahihi kati ya ule wa miaka miwili au wa miaka mitatu na pia kushindwa kuweka wazi kama Singano ni mchezaji huru au bado anamkataba na klabu hiyo.