Saturday , 25th Nov , 2017

Mchezaji Said Hamis Juma maarufu kama Ndemla amefanikiwa kufuzu kwenye majaribio yake ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya. 

Ndemla amefuzu kwenye majaribio yake nchini Sweden kwenye klabu ya Eskilstuna ambapo sasa anatarajiwa kurejea nchini siku ya jumatatu Novemba 28. 

Taarifa ya klabu ya Simba imeeleza kuwa baada ya Ndemla kurejea nchini, klabu za Simba na Eskilstuna zitaanza mazungumzo ya kimkataba ili kumwezesha kiungo huyo kwenda Sweden kwa ajili ya kujiunga na klabu hiyo.

Aidha klabu ya Simba imeeleza kufurahishwa na hatua ya Ndemla kufuzu majaribio hayo huku Simba ikithibitisha kuwa  haitasita kumruhusu mchezaji yoyote anayepata fursa adhimu kama hiyo itakayomsaidia mchezaji binafsi, klabu na Taifa kwa ujumla. 

Simba pia imebainisha kuwa kuelekea mkutano mkuu maalum wa klabu wa tarehe 3-12-2017, itaanza kwa kukutana na viongozi wote wa matawi kwenye makao makuu ya klabu hiyo kuanzia saa nne asubuhi siku ya jumapili ya tarehe 26-11-2017.