Monday , 10th Sep , 2018

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe amempongeza bondia, Hassan Mwakinyo aliyeshinda pambano lake nchini Uingereza wikiendi iliyopita kwa kumchapa, Sam Eggington katika raundi ya pili.

Bondia Hassan Mwakinyo kushoto akiwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe (kulia)

Akijibu swali la mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi hii leo bungeni jijini Dodoma, Waziri Mwakyembe amesema,

“Mhe.Spika niruhusu nielezee kidogo yaliyofanyika usiku wa jana kwa mtanzania mwenzetu Hassan Mwakinyo wa Tanga kwa ushindi mnono aliupata huko Birmingham, Uingereza kwa kumchapa bondia wa Uingereza, Sam Eggington katika raundi ya pili tu kati ya raundi kumi"

“Kabla ya pambano hilo kufanyika, bondia wa Uingereza alikuwa namba nane katika ubora duniani kati ya mabondia 1852 wakati bondia Hassan alikuwa bondia wa 174 na baada ya matokeo haya, Hassan ni bondia wa 16 duniani na ni bondia wa kwanza barani Afrika na Tanzania", ameongeza Dkt.Mwakyembe.

Aidha katika swali la nyongeza la mbunge wa Malindi, Ally Saleh lililouliza kama serikali ilimtambua bondia, Hassan Mwakinyo kabla ya pambano hilo, Waziri Mwakyembe amejibu.

“Mwanamasumbwi, Hassan Mwakinyo sisi kama serikali tulikuwa tunamfahamu kabla ya pambano hilo, alikuwa bingwa wa WBA kwa bara la Afrika na alikuwa nafasi ya 174 kidunia katika uzito wa Welterweight, kwa hiyo tumpongeze kijana huyu"

“Tunahakikisha sasahivi kuwa vijana wetu wote wanaofanya vizuri katika mashindano mbalimbali tunawatambua na kuendeleza vipaji vyao ", amemalizi Dkt.Mwakyembe.