Baadhi ya wabunge, Rais wa TFF wakiwa kwenye picha ya pamoja na wachezaji wa Serengeti Boys, leo bungeni Dodoma
Pia wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekubaliana kuchangia posho zao za kikao cha leo kwa ajili ya kuchangia maandalizi ya timu ya vijana na Serengeti Boys
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ametoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndassa aliyetaka kujua ni lini timu hiyo itaingia kambini kwani umebaki mwezi mmoja pekee kabla ya michuano hiyo kuanza.
Waziri Nape nnauye akiwa na wachezaji wa Serengeti Boys wakati wa mchezo wao dhidiya Congo, mwishoni mwa mwaka jana katika uwanja wa Taifa DSM
"Kama Serikali kwanza nilihakikishie Bunge lako kwamba tumeshiriki kikamilifu kwa wao Serengeti Boys kufanikiwa kufika pale walipofika ikiwemo kutafutia rasilimali kwa wadau na niwashukuru sana wadau wa sekta binafsi ambao wamekuwa wakijitolea kuhakikisha timu hii inafanya vizuri," amesema Nape.
Nape amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta binafsi pia watahakikisha zinapatikana rasilimali za kutosha kuhakikisha vijana hao wanapiga kambi yao lakini pia wanakwenda kuchukua kombe na sio kushiriki.
"Na kila tukiangalia uwezekano wa kushinda ni mkubwa sana, niwaombe wabunge na watanzania kwa pamoja tuungane kwa dua zetu na rasilimali zetu kuhakikisha kwamba Serengeti Boys wanakwenda na wanafanya vizuri na wanarudi na ushindi hapa nchini," amesema Nape.
Michuano ya AFCON kwa vijana inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 21 mpaka Mei 04 mwaka huu nchini Gabon.