Friday , 15th Jul , 2016

Mtanzania Mbwana Samatta alifungia timu yake ya KRC Genk bao la pili, dhidi ya Buducnost ya Montenegro Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk,akicheza mechi ya kwanza katika michuano ya pili kwa ukubwa barani Ulaya.

Mshambuliaji wa Genk, Mtanzania Mbwana Samatta (katikati) akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao dhidi ya Buducnost, michuano ya mchujo Europa League

Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefunga bao lake la kwanza katika michuano ya Europa League usiku huu, timu yake, KRC Genk ikiilaza 2-0 Buducnost ya Montenegro Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.

Samatta, aliyejiunga na Genk mwezi Januari mwaka huu, ameweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mchuano ya ngazi kubwa ya vilabu Barani Ulaya, pia akiweka historia ya kucheza mechi ya kwanza ya Europa na kufunga bao.

Katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Pili ya mchujo, Samatta alifunga bao la pili dakika ya 79, baada ya kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Neeskens Kebano kufunga la kwanza kwa penalti dakika ya 16.

Genk sasa itatakiwa kwenda kuulinda ushindi wake katika mchezo wa marudiano Julai 21, Uwanja wa Pod Goricom mjini Podgorica ili kusonga mbele Raundi ya Tatu ya mchujo.