Saturday , 24th Sep , 2016

Mchezaji Paul Pogba ambaye ni kivutio kikubwa na amekuwa gumzo kwa wachezaji wa timu ya Manchester United, leo amejitoa kimaso maso kwa kuifungia Man U goli la 4 na kuipa ushindi timu hiyo ligi kuu ya England.

Kwenye mechi iliyochezwa leo katika uwanja wa nyumbani Old Trafford dhidi ya washindi wa Premier League msimu uliopita Leicester City, timu ya Manchester Utd imemtandika Leicester City goli 4, huku Leicester ikiambulia goli moja la kufutia machozi lililofungwa na kinda Demarai Gray.

Goli la kwanza la Manchester United lilifungwa na Chris Smalling katika dakika ya 22 ya mchezo, likifuatiwa na la Juan Mata katika dakika ya 37, dakika 3 baadaye Rashford akaifungia Manchester United goli la 3, huku Pogba akaamua kutokubali kushindwa na wachezaji wenzake ili asiambulie tena matusi, na kutandika goli la 4 dakika 2 baada ya Rashford kufunga goli la 3.

Manchester United leo imeandika historia nyingine ya kufunga magoli manne kwa 1 ndani ya kipindi cha kwanza kwenye uwanja wa nyumbani Old Trafford tangu Agosti 2006, ambapo timu hiyo iliitandika Oxford United F.C. magoli 4 kwa 1, yaliyofungwa na Solskjær, Ronaldo na Fletcher, iliyochezwa 'Kassam Stadium'.

Pogba ambaye alivunja rekodi ya kuwa mchezaji aliyenunuliwa kwa bei ghali zaidi duniani, alikuwa hajawahi kuifungia timu yake ya Manchester United tangu imchukue, mwezi Agosti 2016, na hatimaye leo kufuta aibu hiyo.