Mlinzi wa Azam FC Erasto Nyoni amesema, hawajawahi kukutana na timu walizocheza nazo na wamefanya vizuri japo baadhi ya watu wanadhani wameenda kushiriki bonanza lakini wao wanaangalia wanalengo gani na wanatafuta kitu gani cha kuwasaidia katika mashindano yaliyo mbele yao.
Kwa upande wake mlinda mlango wa timu hiyo Ivo Mapunda amesema, mashindano hayo yatawasaidia kwa kuiwakilisha nchi vizuri katika mashindano ya shirikisho pamoja na kuambiwa kama wanashiriki bonanza lakini bonanza hilo ni zuri kwao kwa sababu wanajiandaa na mashindano ya kimataifa na wamekutana na timu zinazoshiriki mashindano ya kimataifa ambazo zitawasaidia kujifunza na kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Naye kiungo wa timu hiyo Frank Domayo amesema, wamekutana na wachezaji wengi wa kimataifa tofauti na Tanzania hivyo hiyo ni fursa kubwa kwao kwa ajili ya kujifunza kutoka kwa timu tofauti.
Kwa upande wake mshambuliaji Farid Mussa amesema, mashindano hayo yatawasaidia kuweza kuwasoma wapinzani wao jinsi ya kucheza kwa nyumbani na ugenini lakini lengo hasa likiwa kufanikisha malengo yao yote ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara pamoja na kombe la shirikisho.
Naye beki chipukizi wa Azam FC, Gardiel Michael amesema, mashindano hayo ni muhimu kwao kwani wanajiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yao na wamejifunza mifumo ya kuweza kucheza na wapinzani wao pamoja na kuendana na hali ya hewa.
Azam FC itashuka tena dimbani siku ya Jumatano dhidi Zanaco FC katika mchezo wao wa mwisho kabla ya kurejea nchini kwa ajili ya muendelezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara.

