Tuesday , 29th Nov , 2016

Ndege iliyobeba watu 81, wakiwemo wachezaji wa klabu moja ya soka ya Chapecoense kutoka nchini Brazil, imeanguka eneo la Medellin nchini Colombia asubuhi ya leo.

Timu ya Chapecoense(kushoto), ikiwa ndani ya ndege, huku juu (kulia) ikionesha ndege hiyo iliyoanguka na upande wa chini na waokoaji wakiwa wamembeba mchezaji wa timu hiyo, aliyenusurika kati ya watu 6 waliopona, Alan Ruschel

Kwa mujibu wa taarifa za polisi kutoka nchini Colombia, Jumla ya watu 76 wamethibitika kupoteza maisha huku watu watano pekee wakinusurika.

Awali watu 7 waliokuwa wameokolewa lakini watu wawili kati yao akiwemo golikipa wa timu hiyo wakafariki baada ya muda mfupi.

Ndege hiyo inayodaiwa kupata hitilafu za mfumo wake wa umeme ilikuwa safarini kutoka Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji wa timu ya Chapecoense, ambao walikuwa wamepangiwa kucheza mechi ya fainali ya Copa Sudamericana, dhidi ya timu ya Medellin, Atletico Nacional, Jumatano hii.

Timu hiyo inayotoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil, ilipandishwa kucheza ligi ya daraja ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014 na ilifika fainali ya kombe hilo la Sudamericana kwa kuilaza San Lorenzo ya Argentina.

Taarifa zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace 146 ambayo imekuwa ikitumiwa na shirika la ndege la Lamia la Bolivia, ilikuwa na abiria 72 na wahudumu tisa.

Hata hivyo, kwa kuwa hakuna moto kwenye eneo hilo la tukio, bado waokoaji wanamatumaini ya kuwapata waathirika wengine.