
Msanii Alikiba
Ali Kiba ameweka wazi furaha yake hiyo leo, ikiwa ni siku moja tu imepita tangu acheze mchezo wa kwanza akiwa na timu yake ya Coastal Union aliyojiunga nayo kwenye dirisha la usajili la mwezi Juni mwaka huu.
''Nina furaha kuanza kukifanyia kazi kitu ambacho nakihusudu sana baada ya muziki wangu. Naishukuru Costal Union kwa kuniamini na kuungana nami kupitia brand yangu ya Mofaya Energy Drink na kunipa fursa ya kuwa sehemu ya timu''. amesema.
Ali Kiba ambaye pia ni mdhamini wa timu hiyo kupitia kinywaji chake cha Mofaya, amesema ushirikiano baina ya pande mbili ambazo ni klabu na yeye mwenyewe, utaleta mafanikio kwa wote.
Mchezaji wa Coastal Union Alikiba (jezi nyekundu)
Nyota huyo ambaye si mgeni kwenye soka kutokana na kiwango chake ambacho amekuwa akikionesha kwenye michezo mbalimbali ikiwemo zile za hisani, amewashukuru mashabiki wake kwa kuunga mkono uamzi wake huo wa kucheza soka la ushindani.
Kutokana na uwezo wake mkubwa katika fani ya muziki na uamzi wake wa kuhamia kwenye soka, unaweza kumfananisha na bingwa wa zamani wa riadha duniani Usain Bolt, ambaye pia ameanza kucheza soka la ushindani baada ya kufanya vizuri kwa muda mrefu kwenye riadha.