Monday , 4th May , 2015

Mzunguko wa pili wa ligi ya mpira wa wavu mkoa wa Dar es salaam inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei tisa mwaka huu katika viwanja vya shule ya msingi Uhuru wasichana pamoja na uwanja wa ndani wa taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, mjumbe wa kamati ya maandalizi na ufundi ya Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es salaam DAREVA, Nassoro Shariff amesema, baada ya kumaliza kozi ya waamuzi iliyoanza Aprili 28 hadi Mei mbili mwaka huu imefungua milango ya ligi hiyo.

Shariff amesema, ligi hiyo ilianza kutimua vumbi Februari 28 mwaka huu kwa kushirikisha vilabu 11 saba vikiwa vya wanaume na vinne vya wanawake ambapo mpaka mzunguko wa kwanza unakamilika, timu ya wanaume ya Tanzania Prisons inaongoza ikiwa na pointi 19, ikifuatiwa na Jeshi Stars yenye pointi 17 huku JKT Stars ikiwa nafasi ya tatu yenye Pointi 14 huku Chui ikiburuza mkia ikiwa haijashinda mechi yoyote.

Kwa upande wa wanawake, Tanzania Prisons inaongoza ikiwa na Pointi tisa, ikifuatiwa na Jeshi Stars yenye Pointi sita huku JKT Stars ikishika nafasi ya tatu ikiwa na Pointi tatu huku Makongo ikiburuza mkia ikiwa haina Pointi hata moja.