Tuesday , 23rd Dec , 2014

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoani Mbeya MREFA, kimewataka viongozi wa vilabu vya soka mkoani humo kuacha suala la vurugu katika mechi za Ligi Kuu mzunguko wa pili zinazotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 26, 2014 katika viwanja mbalimbali nchini.

Akizungumza na East Africa Radio, katibu mkuu wa MREFA, Suleiman Haroub amesema wamekutana na viongozi wa timu mbili zilizopo mkoani humo ambazo ni Tanzania Prisons na Mbeya City ambapo wamewapa maelezo yote ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha viongozi hao sheria wanazotakiwa kufuata katika soka.

Haroub amesema katika mechi mbalimbali za Ligi kuu zilizopita kumekuwa na baadhi ya wachezaji na viongozi kuanzisha vurugu pale wanapoona wameonewa bila kufuata sheria ambazo zingeweza kuwasaidia ili kuweza kupata haki.

Haroub amesema timu yoyote itakayobainika kuwa chanzo cha vurugu itachukuliwa hatua kali ambayo anaamini itakuwa ni fundisho kwa timu nyingine shiriki za ligi hiyo mkoani humo.