Wachezaji wa Manchester United na Chelsea kwenye mechi ya leo.
Katika mchezo huo ulioanza mchana na kumalizika jioni hii, ulishuhudiwa Chelsea wakitangulia kwa bao moja la Antonio Rudiger kabla ya Anthony Martial kusawazisha na kuongeza bao la pili, hivyo kutaka kurudia 'Come back' ya Oktoba 6 walipowafunga Newcastle United 3-2 wakitokea nyuma kwa mabao 2-0.
Hata hivyo rekodi hiyo ikazuiliwa na Ross Barkley ambaye aliisawazishia Chelsea dakika za mwisho za mchezo, hivyo mechi kumalizika kwa kugawana alama 1.
Katika mchezo huo Mfaransa Martial amekuwa mchezaji anayeongoza kwa mabao mengi ndani na Man United kwa wachezaji waliopo tangu mwaka 2015 alipocheza mechi yake ya kwanza. Amefunga mabao 39 katika michuano yote.
Pia imekuwa mara yake ya kwanza kufunga mabao 2 kwenye mchezo mmoja tangu alipofanya hivyo kwa mara ya mwisho Novemba 2016 dhidi ya West Ham.
Bao la Ross Barkley (90 +6), limekuwa bao la kuchelewa zaidi kufungwa Man United kwenye EPL, tangu walipofungwa bao la aina hiyo na David Ngog wa Liverpool October 2009 katika dakika ya 90:27.
Chelsea inaweza kudondoka hadi nafasi ya pili ikiwa na alama 21 endapo Man City watashinda dhidi ya Burnley leo. Man United wao wamefikisha alama 14 katika nafasi ya 9.


