
Kocha msaidizi wa mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Young Africans, Charles Boniface Mkwasa amesema kikosi chao bado kina tatizo la kutokuwa makini kuhakikisha wanamiliki mpira na kufanya mashambulizi ya haraka na kukosa umakini wa kuchukua mpira kwa haraka pindi wanapopoteza.
Mkwasa ambaye pia ni kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars, amesema tatizo hilo amelibaini kwenye mchezo wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba Septemba 26 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ambapo amesema tatizo hilo watalifanyia kazi kabla ya michezo inayofuata.
Yanga ilionekana ikikosa kujiamini hasa katika dakika 20 za mwanzo za mchezo dhidi ya Simba na iliwafanya wapinzani wao kutawala mechi hiyo kwa dakika hizo hadi pale ilipokuja kupata bao dakika 1 kabla ya mapumziko na kipindi cha pili kucheza kwa kujiamini zaidi na kupata bao la pili lililoivunja nguvu Simba.
Yanga ipo kileleni kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 12 ikifuatiwa na Azam FC nayo ikiwa na pointi 12 ambapo mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Jumatano wana kibarua kigumu dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro.