Monday , 3rd Aug , 2015

Mlinda mlango wa Mabingwa wa Kombe la Kagame, Timu ya Azam FC Aishi Manula amesema, sababu za Kocha wa Timu hiyo Stewart Hall kuona mapungufu katika kikosi hicho ni kutokana na kuwa na muda mchache wa kupokea na kuelewa mfumo mpya wa kocha wao.

Akizungumza na East Africa Radio, Manula amesema, kocha huyo wakati kaanza kukinoa kikosi hicho wachezaji wengi walikuwa wakiitumikia Timu ya Taifa hivyo tangu wachezaji wa timu ya Taifa walipoungana walijitahidi kuelewa mfumo huo mpya na kuufanyia kazi japo kidogo lakini wamefika pale walipokuwa wakipatarajia na wanaamini watafanya vizuri kwani bado wananafasi ya kumuelewa kocha zaidi.

Kwa upande mwingine Manula amesema, kipaji alichonacho atazidi kujifunza anapokuwa na watu tofauti na hata asipopata nafasi ya kukitumikia kikosi cha timu ya Taifa kwa upande wake hataweza kujisikia vibaya kwani ni nafasi pia ya kuendelea kujifunza anapokuwa au asipokuwa na kikosi hicho na atakapopata nafasi ataonyesha kile watanzania wanachokihitaji.

Azam FC ilitwaa ubingwa wa Kombe la Kagame hapo jana aada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya bao 2-0 yaliyofungwa na nahodha wake John Raphael Bocco ‘Adebayor’ na Kipre Herman Tchetche katika mchezo wa fainali uliofanyia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika michuano hiyo, Azam FC imejiwekea rekodi nzuri ya kutokuruhusu goli hata moja kupenya katika nyavu zake ndani ya Dakika 90 ya mchezo huku beki muhimili wa ukuta wa timu hiyo, Serge Wawa Paschal akiwa imara kuzuia hatari katika timu yake ikichangiwa na uimara wa mlinda mlango Aishi manula.