Tuesday , 23rd Jun , 2015

Nchi alikwa za Zambia, Malawi, Burundi, Uganda na Kenya na wenyeji Tanzania zimehakiki ushiriki wa mashindano ya taifa ya wazi ya Tenisi Tanzania yanayotarajiwa kuanza hapo kesho Uwanja wa Gymkhana jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, msimamizi wa mashindano hayo Salum Mvita amesema, mpaka sasa wanawachezaji 60 lakini wanatarajia kuwa na wachezaji zaidi ya 100 ambapo yatashirikisha wachezaji wa nchi mbalimbali waishio Tanzania zikiwemo nchi za Cameroon, Marekani na Uingereza.

Mvita amesema, upinzani utakuwa mkubwa katika mashindano hayo kutokana na kila timu kujiandaa ambapo mashindano hayo yatashirikisha wachezaji vijana na wazee na watacheza mmoja mmoja na wawili wawili.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mashindano hayo, Omary Abdallah China amesema kwa upande wake amejiandaa vizuri na anaamini ushindi utabaki Tanzania kutokana na maandalizi aliyofanya mapema.

China amesema, mchezo huo unawachezaji wengi kwa upande wa Tanzania na wanapata taarifa mapema juu ya mashindano lakini wengi wamekuwa wavivu kufanya mazoezi suala linalochangia wanamichezo wa mchezo huo kushindwa kushiriki mashindano hayo.