Friday , 20th Jul , 2018

Tetesi zinaeleza kwamba mabingwa wa soka Afrika Mashariki na kati, Azam Fc wako mbioni kumrejesha mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo, Kipre Tchetche kwaajili ya msimu ujao wa ligi kuu Tanzania bara.

Mchezaji Kipre Tchetche aliyeinua mikono juu akiwa kwenue jezi za klabu yake ya sasa Terengannu.

Tchetche anayecheza katika klabu ya Terengannu inayoshiriki ligi kuu nchini Malaysia anatajwa kurejea katika klabu hiyo muda wowote baada ya Mkurugenzi wa Azam Fc, Yussuph Bakhresa kuelekea nchini humo kukamilisha usajili wake.

Kipre Tchetche amebakiza miezi mitatu katika mkataba wake na Terengannu, taarifa zinaeleza kuwa Mkurugenzi huyo wa Azam Fc yuko katika mazungumzo na uongozi wa klabu yake ili waruhusiwe kumsajili.

Juhudi za kumtafuta Afisa habari wa Azam Fc, Jaffar Idd Maganga kuzungumzia tetesi za usajili huo hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopokelewa mara kadhaa.

Azam Fc ilimnasa Kipre Tchetche na ndugu yake Kipre Balou kwa mara ya kwanza katika michuano ya CECAFA Challenge Cup mwaka 2010, walipokuja na timu yao ya taifa ya Ivory Coast na baadae mwaka 2016 wote waliondoka kuelekea nchini Oman .

Nchini Oman, Kipre Tchetche alichezea klabu ya Al-Suwaiq kabla ya kuelekea Malaysia kwenye klabu anayoichezea sasa ya Terengannu, huku ndugu yake, Kipre Balou akiichezea klabu ya Fanja Sc mpaka sasa.