Kipa namba moja wa timu ya Mtibwa Sugar Said Mohammed Nduda
Ndunda aliyekuwa nje ya Uwanja tangu mwanzoni mwa msimu wiki hii ameanza mazoezi kikamilifu na wachezaji wenzake wakati timu ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Toto Africans utakaopigwa leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
“Nimepona na nimerudi tena uwanjani na nimeanza mazoezi kikamilifu na wachezaji wenzangu,”amesema Ndunda.
Kipa huyo wa zamani wa Yanga na Maji Maji amesema anahamu ya kurejea uwanjani kuisaidia timu yake baada ya kuwa nje ya Uwanja kwa muda mrefu.
Pamoja na hayo, Ndunda amewapongeza wachezaji wenzake kwa kuipigania timu yao vizuri tangu mwanzo mwa msimu hadi kuifanya iwe ndani ya tano bora kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
“Timu ipo katika nafasi nzuri, ipo nafasi ya nne maana yake hata sisi tumo kwenye mbio za ubingwa, kwa kweli nawapongeza wachezaji wenzangu na benchi zima la ufundi, na mimi sasa naungana nao kuongeza nguvu,”amesema Ndunda.
Mtibwa Sugar inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwa pointi zake 17 ilizokusanya kwenye mechi 12, ikishinda nne, sare tano na kufungwa tatu.





