
Kili Stars iliyo chini ya kocha Abdallah Kibadeni inahitaji ushindi mwingine ili kusonga mbele katika michuano hiyo inayoendelea Addis Ababa nchini Ethiopia.
Matokeo ya jana yanaifanya Kili Stars ianzie kileleni mwa Kundi A ikiwashusha Rwanda walioifunga Ethiopia 1-0 katikia ufunguzi wa michuano hiyo iliyoanza Novemba 21.
Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ amefunga mabao mawili katika ushindi huo, moja kwa penalti dakika ya 12 baada ya beki wa kulia, Shomary Kapombe kuangushwa na lingine dakika ya 54.
Mshambuliaji Elias Maguri naye akafunga mabao mawili dakika ya 17 na 66 kukamilisha kipigo cha bao nne.
Kipa Aishi Manula aliyeanza katika katika mchezo huo alifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo mingi ya hatari langoni mwake na kujizolea sifa kemkem.
Kikosi cha Tanzania Bara leo kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kevin Yondan, Salum Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Malimi Busungu dk71, Said Ndemla, Johm Bocco, Elias Maguri na Deus Kaseke.