Tuesday , 30th Jan , 2018

Katika mwendelezo wa michuano ya kombe la shirikisho klabu ya Azam FC, imetoa kipigo kikubwa cha mabao 5-0 dhidi ya timu ya Shupavu FC ya mkoani Morogoro kwenye mchezo uliomalizika jioni hii.

Azam ambayo imekuwa na utamaduni wa kuwaamini vijana katika kikosi cha kwanza imeshuhudiwa leo nyota chipukizi wa timu hiyo Paul Peter akiibuka shujaa baada ya kufunga mabao matatu (Hat-trick) katika ushindi huo wa 5-0.

Paul Peter amefunga mabao hayo katika kipindi cha pili akiwa ameingia kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mbaraka Yusuf. Amefunga dakika za 52, 77 na 88.

Matokeo hayo sasa yanaifanya Azam itinge hatua ya 16 bora ya michuano hiyo ya Shirikisho Tanzania (FA) ambapo sasa itasubiri mechi zingine za leo zimalizike kabla ya droo kuchezeshwa na kujua watakutana na timu gani.

Mabao mengine ya Azam FC leo yamefungwa na nyota wengine Yahya Zayd dakika ya 45 huku Iddi Kipagwile akifunga bao la pili kwenye dakika za majeruhi kipindi cha kwanza.