Wednesday , 2nd Sep , 2015

Mshambuliaji Gaudence Mwaikimba ameiadhibu timu yake ya zamani, Azam FC akitoa mchango mkubwa kwa timu yake mpya, JKT Ruvu kushinda mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika hapo jana uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, ambao kocha Muingereza Stewart Hall aliwakosa nyota wake wa kikosi cha kwanza walio na timu za taifa, JKT Ruvu walipata bao la kwanza dakika ya 10 Mwaikimba akimalizia shuti la Mussa Said akitumia makosa ya kipa Mwadini Ali ambapo bao hilo halikudumu sana, kwani Azam FC walisawazisha kupitia kwa Kipre Herman Tchetche dakika tano baadaye, akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya JKT.

JKT Ruvu inayofundishwa na beki wa zamani wa Yanga SC, Freddy Felix Minziro ilipata bao lake la ushindi dakika ya 85 mfungaji Najim Magulu aliyemalizia pasi ya Mwaikimba baada ya beki Bryson Raphael kuchanganyana na kipa wake Mwadini Ali.

Mchezo huo ulikuwa maalum kwa timu zote kujiandaa na ligi kuu ya soka Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi wiki ijayo.