Thursday , 13th Oct , 2016

Jeshi la Polisi Tanzania limesema lipo tayari kukabiliana na vikundi vinavyoibuka mitaani kwa majina mbalimbali na kutishia usalama wa raia na mali zao kwani hiyo ndiyo kazi yao kubwa.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania ACP Advera Bulimba

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania ACP Advera Bulimba katika kipindi cha KIKAANGONI kinachorushwa na ukurasa wa facebook wa EATV wakati akijibu maswali ya wananchi kuhusiana na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini.

“Makundi ya Panya Road na Black Mamba tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana nayo na tunawahakikishia wananchi kwamba tupo imara kukabiliana nayo kinachotakiwa ni kupata taarifa sahihi kutoka kwa wananchi na sisi tutazifanyia kazi haraka iwezekanavyo” Amesema

Aidha ACP Bulimba amesema askari polisi wanapomkamata raia kisheria hawampigi au kutumia nguvu bali inapotokea viashiria kwamba mtu aliyekamatwa anakaidi amri ya polisi. kisheria wanaruhusiwa kutumia nguvu kulingana na hali halisi inayojitokeza.

Pamoja na hayo ACP Bulima amewataka wananchi kuendelea kutii sheria bila shuruti na kutoa taarifa zitakazosaidia jeshi hilo kufanya kazi yake ya kuhakikisha usalama unakuwepo katika makazi ya watu, maeneo ya biashara pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.