Friday , 28th Oct , 2016

Katibu Mkuu wa CHADEMA Dkt. Vincent Mashinji amesema Umoja wa Katiba  ya Wananchi UKAWA kwa sasa wanamuita Prof Ibrahim Lipumba ‘Bwana Yule’

Prof. Lipumba

Hiyo ni baada ya kuona amekiuka malengo na mikakati ambayo walikuwa wameiweka kwa pamoja na kuanza kuwagawa wana umoja huo.

“Sisi UKAWA tunamwita Prof Lipumba bwana yule, maana hatujui yupo nyuma ya nani na ana  lengo gani kwa sababu kwa taaluma yake na  haiba yake na anavyofanya sasa hivi haieleweki kabisa” Amesema Dkt. Mashinji

Pamoja na hayo Dkt. Mashinji aliyekuwa KIKAANGONI ya EATV, amesema UKAWA ipo palepale na itaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kwamba demokrasia ya kweli inapatikana nchini.

 

Dkt. Vincent Mashinji

Kuhusu madai kuwa CHADEMA inaingilia masuala ya CUF, Mashinji amesema siyo kweli kuwa CHADEMA inaingilia masuala ya ndani ya chama hicho, ndiyo maana haikushiriki kikao chochote cha CUF, lakini inachofanya ni kushauri kuhusu maamuzi ambayo yamekwishaamuliwa na vikao halali vya CUF kama mwanafamilia wa UKAWA.

Aidha Dkt. Mashinji ameongeza kuwa Katiba ya wananchi ambayo ilikwama inatakiwa kufanyiwa kazi upya na hatimaye kuifanya ikubalike kwa kuwa ndiyo suluhisho la mambo mengi yanayoendelea nchini na bila hiyo bado mambo yatazidi kuenda kama tulikotoka.