Tuesday , 20th Oct , 2015

Mwanahabari wa habari za burudani na mtayarishaji wa muziki Fredrick Bundala, amewashauri wasanii ambao wamefanikiwa kupitia muziki kuwekeza katika sekta nyingine, ili kuweza kulinda heshima yao hapo baadae.

Fredrick Bundala ameyasema hayo alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo kinachorushwa na East Africa Radio, na kueleza kwamba muziki ni kitu cha msimu hivyo ni lazima wakumbuke kujiwekea akiba ya kesho.

"Nawashauri wasanii walio juu sasa hivi, kwa sababu muziki ni kitu cha msimu hauwezi ukaheat muda wote, hauwezi uka heat muda wote, kwa hiyo wakumbuke kwamba fedha ambazo wanazipata sasa hivi wanatakiwa waziwekeze, kwa kufanya biashara za kawaida ama biashara ambazo zina uhusiano na muziki", alisema Fredrick.

Pia Fredrick Bundala amesema wasanii wengi wamekuwa wakijisahau na kufanya starehe ambazo zinawashusha kiuchumi, huku akiwatolea mfano baadhi ya wasanii ambao walifanya vizuri hapa nyumbani miaka ya nyuma, lakini kwa sasa wamepotea kimuziki na kiuchumi pia.

"Ukiangalia kwa mfano, historia inaonyesha kabisa wasanii wengi ambao waliwahi kufanya vizuri sana zamani, na sasa hivi hawafanyi vizuri, ni kwa sababu walijisahau wakalewa na umaarufu wakadhani kwamba ule umaarufu utaendelea kuwepo, kwa maana kwamba walipata fedha nyingi sana lakini wakawa wanazitumia vibaya, hawawekezi, wakiwa na matumaini kwamba watapata fedha zingine baadae", alisema Fredrick.