Monday , 17th Feb , 2014

Msanii wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu leo hii amekana shtaka la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake nyota wa filamu Marehemu Steven Kanumba, katika shauri lililosomwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika maelezo ya awali yaliyosomwa na wakili wa serikali Monica Mbogo, mbele ya Jaji Rose Temba anayesikiliza shauri hilo, yamesema siku ya tukio kulikuwa na ugomvi kati ya marehemu na mshitakiwa, na baadae usiku wa saa sita mshtakiwa Lulu aliondoka baada ya marehemu Kanumba kuanguka chumbani, ambapo alfajiri ya saa 11 alikamatwa akiwa Bamaga.

Kwa upande wake wakili anayemtetea Lulu, Peter Kibatala amesema wameridhishwa kwa sehemu kubwa na maelezo ya awali ya mteja wao, ambapo kesi hiyo imeahirishwa mpaka itakapopangwa tena huku kila upande ukitakiwa kuleta mashahidi watatu.