Sunday , 9th Apr , 2017

Mwanamuziki wa nyimbo za Injili Emmanuel Mbasha amefunguka kuwa aliyekuwa mke wake (Flora) alilazimika kuacha uimbaji wa kwaya na kuamua kuimba kama muimbaji wa kujitegemea baada ya kumshauri afanye hivyo.

Akiwa Kikaangoni kwenye ukurasa facebook wa EATV Jumatano iliyopita, Mbasha amesema lengo la kumshauri afanye hivyo ni ili kuweza kumuongezea nguvu kwa kushirikiana naye ili waweze kuwa watumishi wakubwa wa Mungu katika huduma ya uimbaji kwa kuwa na yeye alikuwa ni mwanamuziki wa bongo fleva kabla ya kuokoka.

"Mwanzo nilikuwa naimba bongo fleva kina marehemu Ngwear, Mez B na wengine wa Chemba Squad  nilikuwa naimba nao kipindi hicho lakini nilikuja kuokoka nikaacha, ilipofika wakati wa kuoa nikakutana na Flora ambaye alikuwa mwanakwaya kanisani nilimshauri aimbe kwa kujitegemea na mimi nilikuwa nyuma yake kuhakikisha namtengenezea mistari mizuri na vingine vingi kama mume nilikuwa nahakikisha vinaenda sawa na hata kuvaa nilikuwa nasimamia mimi mwenyewe" Aliongeza Mbasha.

Aidha Mbasha ameongeza kuwa hata baada ya kuachana na Flora bado anaendelea kuimba kwa sababu ni kitu anachokipenda na anaamini watu wengi wanabarikiwa kupitia uimbaji wake na hata yeye anafarijika kwenye moyo wake ingawa pengo la Flora linaonekana.

Emanuel Mbasha

Kuhusu yeye kuonekana kuwa 'smart' wakati wote, amesema kuwa anaimba nyimbo za injili hivyo si busara kuonekana mchafu kwani hata mbele za Mungu ukiimba ukiwa msafi inapendeza na kuvutia.

"Mimi kupendeza napenda, napenda kuwa smart lakini hata hivyo kama mtumishi wa Mungu yapasa kuwa smart mbele za watu, inapendeza sana, na kupendeza ni gharama sana na nipo tayari kujigharamia kwa sababu najipanga kwa kipato ninachokipata" aliongeza Mbasha.

Kuhusu taarifa za Flora kuolewa, Mbasha amesema hajui chochote kwa sasa kuhusu Flora, huku akiweka wazi kuwa hatakuwa tayari kuhudhuria harusi ya Flora kwa sasa endapo ataalikwa

"Kama nikipewa mualiko kwenda kwenye harusi ya Flora kwa sasa, sitakwenda"