Kwenye ukurasa wake wa instagram Nonini amesema kutokana na ukongwe alionao Eddie kwenye tasnia ya filamu nchini humo na hata Hollywood, alistahili sifa zaidi na si kama wanavyofanya kwa Lupita.
“Lupita amefanya filamu mbili na kwa hilo limewafanya Wakenya wafurahi na kujivunia kuwa na mmoja wao kwenye Hollywood, lakini hivi Wakenya wamshawahi kumsikia Eddie Mua Gathegi? Ni Mkenya ambaye yuko zaidi ya miaka 15 Hollywood, Eddie ni muigizaji wa kipekee mwenye kipaji ambaye anastahili kutambuliwa nyumbani, alifanya vizuri zaidi hususan kwenye The Black list, criminal activities na The Twilight”, alisema Nonini.
Wakimtetea Lupita Nyong'o ambaye anazidi kuja juu kwenye anga za Hollywood kutoka Kenya, mashabiki wake wamesema umaarufu hauji na wingi wa filamu ulizofanya, bali ni ubora wa filamu iliyoigizwa, hivyo Gathegi huenda akawa ameigiza filamu nyingi huko Hollywood, lakini hiyo haipandishi hadhi ya mtu.
Muigizaji Eddie Gathegi ni Mkenya aliyezaliwa Eastlands Nairobi miaka 36 iliyopita, na kukulia nchini Marekani jimbo la California, na amehusika kwenye filamu nyingi ambazo zinafahamika na wengi kama Blacklist, X Men, Twilight, Aloha na House.


