Tuesday , 4th Oct , 2016

Wasanii wa Muziki na Filamu wametakiwa kuendelea kujitokeza kuchukua fomu za kuwania tuzo za East Africa Television, zinazotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es salaam.

Sophia Mng'anya, Mratibu wa vipindi EATV

Wito huo umetolewa na mratibu wa vipindi vya EATV Sophia Mng'anya alipokuwa akizungumza kwenye jukwaa la sanaa ambalo huendeshwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) katika ofisi za baraza hilo zilizopo Buguruni Dar es Salaam, na kushirikisha wasanii mbalimbali.

Sophia amesema kuwa tuzo hizo zinasaidia kuongeza thamani ya kazi ya msanii kwa kuzidi kumuongezea mashabiki, na pia haziangalii sanaa ya aina moja pekee bali zinaangalia wasanii wa muziki pamoja na filamu.

"Tuzo hizi haziangalii tu sanaa ya aina moja, kwa kuanzia tutaangalia muziki na filamu, kwa hiyo wasanii wa muziki wasanii wa filamu ambao wamefanya vizuri mwaka huu, watatunukiwa nishani zao, kama wasanii bora, kama waigizaji bora, kitu ambacho ningependa wakitilie maanani, tuzo inaipa thamani kazi ya sanaa, inaongeza thamani kwa msanii mwenyewe", alisema Sophia.

Sophia aliendelea kutolea maeleze juu ya tuzo hizo na kusema ....."Unapokuwa nominated kuwa mmoja wa watakaowania tuzo fulani thamani yako inapanda, kwa maana inaongeza wigo wa mashabiki, inaongeza kujulikana kwako na kujulikana kwa kazi yako, na ikumbukwe ni tuzo za Afrika Mashariki, kwa sababu EATV LTD ipo Tanzania, Kenya na Uganda, kwa hiyo tuzo hizi zitahusisha sanaa ya muziki na filamu kwa nchi zote Tanzania, Kenya na Uganda, kwa hiyo wasanii wajitokeze zaidi kuchukua fomu na kushiriki", alisema Sophia Mng'anya.

Sophia amesema watatoa jumla ya tuzo 10 kwa wasanii kutoka Afrika Mashariki ambapo kwa upande wa wasanii wa muziki zitatoka jumla ya tuzo sita, kwa upande wa filamu tuzo tatu huku tuzo moja ikiwa ya heshima.

Tags: