Friday , 31st Aug , 2018

Msanii wa filamu bongo ambaye pia ni mchekeshaji maarufu Steve Nyerere, amesema Barnaba ni miongoni mwa wasanii waliokuwa na kipaji kikubwa katika uimbaji huku akidai tatizo linalomfanya ashindwe kuonekana ni kutojua kuvunja nazi.

Barnaba upande wa kushoto, akiwa na Steve Nyerere (kulia)

Steve ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza kwenye kipindi cha eNewz kinachorushwa na tinga namba moja kwa vijana EATV, na kusema kuwa ni lazima ampe sifa zake licha ya kuwa anamkera kwa tabia yake kushindwa kuloga 'kuvunja nazi' na kubakia kufuga rasta. 

"Barnaba ni msanii mzuri na ndio mtu pekee aliyeweza kufanya 'show' kwenye ndege, hakuna msanii mwingine ila tatizo lake ni moja tu hawezi 'kupiga nazi' yaani hawezi kuloga, yeye kazi yake ni kufuga rasta tu", amesema Steve.
 
Pamoja na hayo, Steve ameendelea kwa kusema "nataka kumwambia Barnaba maisha ni sanaa, Mungu amempa kipaji cha sanaa afanye sanaa kama ajira na asifanye sanaa hii kama 'fashion show'  ili kuburudisha watu.Msema kweli ni mpenzi wa Mungu, Barnaba anakosea kwa sababu hajitambui anajitambua siku ya uzinduzi tu kuvaa vizuri na kupiga poda kidogo".

Kwa upande mwingine, Steve amemtaka Barnaba ajifunze na kujitambua kuwa maisha ya sanaa ni ajira kama zilivyokuwa ajira nyingine, ambazo vijana wamejiajiri kwani akiiheshimu na yeyewe itamuheshimu.