Friday , 26th May , 2017

Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeanzisha dawati la wepesi wa kufanya biashara ambalo lina jukumu la kuondoa ugumu wa kuanzisha na kuendesha biashara  nchini.

Waziri Charles Mwijage

Hayo yamesemwa leo Bungeni na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Magomeni Mhe.Jamal Kassim Ali.

Aidha Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wa kitanzania ili kuwekeza kwenye viwanda hapa nchini.

Miongoni mwa Mikakati hiyo ni Mafunzo yanayotolewa kwa watanzania wenye nia ya kuwekeza katika viwanda juu ya kuibua mawazo ya kibiashara, kuanzisha ,kuendesha na kusimamia biashara kupitia SIDO,kutoa ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuchagua teknolojia sahihi inayoendana na wazo la ujenzi wa kiwanda alilonalo Mtanzania kupitia TIRDO, TEMDO na CAMARTEC na namna ya kupata ama kukuza mtaji wa ujenzi wa viwanda kupitia NEDF, SIDO na TIB.

Pamoja na hayo Wizara imeandaa mwongozo kwa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutenga maeneo ,kusimamia sheria, kanuni, taratibu na kutoa maelekezo kwa wawekezaji.

"Watanzania wanaaotaka ama walio na mitaji mikubwa wanaweza kuwekeza kupitia maeneo ya EPZA ambayo yametengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi, Pia wanaweza kuwasiliana na TIC kupata vivutio mbalimbali vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji,Alisisitiza Mhe.Mwijage.