Thursday , 2nd Jun , 2016

Watu wapatao milioni 4.6 nchini Burundi hawana uhakika wa chakula, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula WFP.

Baadhi ya Wakimbizi kutoka Burundi

Katika taarifa iliyotolewa jana, WFP imeeleza kwamba mzozo wa kiuchumi na kijamii unaoikumba nchi hiyo umezorotesha zaidi hali ambayo tayari ilikuwa dhaifu, kutokana na umaskini na matokeo ya El-nino yakiwemo mvua kubwa na mafuriko yaliyoharibu mavuno.

WFP imeongeza kwamba watu zaidi ya 500,000 wanahitaji msaada wa chakula wa dharura, huku akiba za chakula zikiwa zimepunguwa.

Aidha WFP imetoa wito wa ombi la dola milioni 57 kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa Burundi zaidi ya 265,000 waliotafuta hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Rwanda, Uganda na Tanzania, ikisema kwamba watu 1,000 wanaendelea kuwasili kila wiki.